25 Oktoba 2012 - 05:07

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Kiarabu Bw. Lakhdar Brahimi amesema Serikali ya Syria na baadhi ya viongozi wa waasi wamekubali kusimamisha mapambano wakati wa mapumziko ya siku nne ya sikukuu ya Eid el Hajj, yanayoanza Ijumaa hii.

ABNA- Akieleza Bw. Ibrahimi: "Serikali imekubali kusimamisha mapambano wakati wa sikukuu ya Eid el Hajj, nafikiri serikali ya Syria itatoa taarifa kuhusu kukubali kusimamisha mapambano leo au kesho. Na wengi wa viongozi wa baadhi ya makundi ya waasi tuliowasiliana nao, pia wamekubali kusimamisha mapambano. Kama pendekezo hili litafanikiwa na kufuatwa, tutaweza kuanzisha mazungumzo kuhusu usimamishaji wa mapambano wa muda mrefu zaidi."

Hata hivyo Brahimi hakusema usimamishaji huo wa mapambano utasimamiwa vipi. Taarifa hiyo ya Bw Brahimi imekuja wakati serikali ya Syria inapoyashambulia kutoka angani maeneo yanayodhibitiwa na waasi yaliyo karibu na mji wa Aleppo. Umoja wa Mataifa umepongeza usimamishaji huo wa mapambano ukizitaka pande husika za kikanda na kimataifa zitumie ushawishi wao kuhimiza utekelezaji wa usimamishaji huo wa mapambano. Serikali ya China pia imeeleza kuunga mkono usimamishaji huo wa mapambano.

Wakati huohuo, mashambulizi yameendelea kutokea mjini Damascus na kusababisha vifo na majeruhi. Hapo jana gari lililotegewa mabomu lililipuka katika kitongoji cha mji huo na kusababhosha vifo vya watu 6 na kuwajeruhi wengine 20. Kundi la waasi la al-Ansari limetangaza kuhusika na shambulizi hilo.